Wasiliana nasi | MMM | Barua Pepe |

ZAIDI YA WANANCHI 2500 WAFIKIWA NA HUDUMA ZA KIBINGWA NA BOBEZI MBEYA RRH

Posted on: May 8th, 2025


Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Nyanda za Juu Kusini iliyodumu kwa siku tano, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya,  imetamatika leo Ijumaa Mei 9, huku watu zaidi ya 2500 wakiwa wamehudumiwa kupitia huduma Mkoba.


Mapema leo Mei 9, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Dkt.  Abdallah Mmbaga akizungumza na Madaktari bingwa hao ametoa shukrani kwa kujitoa kwao kuwahudumia wananchi  pamoja na kuwajengea uwezo watumishi mbalimbali wa ngazi za chini katika utoaji huduma.



Amenukuliwa akisema "Kwa niaba ya watumishi na uongozi wa Mbeya RRH, niwashukuru kwa kuwajengea uwezo watumishi pamoja na kujitoa kwenu katika kuhakikisha tunafanikisha zoezi hili, tunaheshimu mchango wenu"


Amesema kumekuwa na wastani wa watu zaidi ya mia tano (500+) sawa na hesabu ya watu zaidi ya 2500 kwa siku tano za Kambi hiyo.


Kwa niaba ya Madaktari Bingwa Dkt. Msafiri Birigi,  kutoka Hospitali ya Kanda Mbeya,  amepongeza maandalizi yaliyofanyika na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, pamoja ushirikiano ambao watumishi wa hospitali hii wameonesha ikiwemo utayari wao katika kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali yao ya utaalamu.


Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni kukosekana kwa kipimo cha uchunguzi wa mfumo wa chakula (endoscopy) hali iliyolazimu baadhi ya wagonjwa kwenda kufanyiwa Hospitali ya Kanda Mbeya, hivyo ushauri ukatolewa kwa uongozi wa Hospitali kuchukua hatua muhimu za kuwezesha upatikanaji wa vipimo na uchunguzi katika eneo hilo.


Dkt. Gilbert Kwesi ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, na Daktari Bingwa wa Upasuaji ameshauri kuimarishwa kwa mawasiliano miongoni mwa viongozi na watumishi wa hospitali hiyo ili kuendelea kuboresha utoaji huduma katika Hospitali hiyo.



Wakati huo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea Magafu Majura amesema uwepo wa Kambi hizi za Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi unasaidia kuimarisha uhusiano na kujengeana uzoefu mahali pakazi miongoni mwa wataalamu wa Afya, hivyo akashauri maeneo yenye uhitaji mkubwa katika maeneo ya Kanda hiyo utengenezwe utaratibu wa kuwa na Kliniki za wiki kwa wataalamu hao kutoka Hospitali zinazounda ukanda huo kuzunguka katika maeneo hayo.



Dkt. Mmbaga, ameahidi kuyafanyia kazi maoni yaliyopendekezwa na madaktari bingwa hao, pamoja na kuendeleza ushirikiano uliopo miongoni mwa Hospitali hizo.


Kambi hiyo ilijumuisha madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Njombe, Songea, Songwe na Mbeya na kwa maeneo yaliyohitaji wataalamu wanaokosekana kwenye hayo maeneo Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Hospitali ya Taifa Muhimbili walileta wataalamu hao.



Miongoni mwa maeneo ambayo wananchi wamenufaika na Huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi katika kambi hiyo ni Upasuaji wa Jumla, Upasuaji wa Mifupa, Magonjwa ya wanawake na Uzazi, Magonjwa ya Ndani, Matibabu na Upasuaji wa Pua, Koo na Sikio, Huduma za Kibingwa za Watoto, Dawa za Usingizi na Ganzi, Radiolojia, Huduma za Kibingwa za Usikivu, Macho, Kinywa na Meno, Upasuaji wa Uso na Taya.