Wasiliana nasi | MMM | Barua Pepe |

WAUGUZI MBEYA RRH WAADHIMISHA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI KWA MATEMBEZI NA MATENDO YA HURUMA

Posted on: May 12th, 2025


Mbeya, Mei 12, 2025 — Katika kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani, wauguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya (Mbeya RRH) wamefanya matembezi maalum ya hamasa na kutoa huduma za huruma kwa jamii ikiwa ni sehemu ya shughuli zao za kijamii na kitabibu.


Maadhimisho hayo yameanza kwa matembezi ya amani kutoka Kabwe stendi hadi hospitalini.


Baada ya matembezi, wauguzi walitembelea wagonjwa waliolazwa wodini na kutoa huduma za huruma ikiwa ni pamoja na kuwafariji, na kuchangia Damu.


Muunguzi Mfawidhi wa hospitali, Bi. Maridhia Mvungi, alisema kuwa maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kutambua mchango mkubwa wa wauguzi katika mfumo wa afya na kuwaenzi wale wanaotoa huduma kwa moyo wa kujitolea.


"Leo tunasherehekea kazi ya wauguzi ambao ni uti wa mgongo wa sekta ya afya. Tunaendelea kuhamasisha upendo, huruma, na huduma bora kwa kila mgonjwa," alisema Bi. Mvungi.


Kwa kipekee Mganga Mfawidhi Dkt Abdallah Mmbaga, ambae alikuwa mgeni Rasmi katika siku ya Wauguzi kwenye hafra iliyofanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya amewapongeza Wauguzi kwa kuendelea kuwa kiongo Muhimu katika kufanikisha huduma bora kwa Wananchi wanaokuja kupata huduma katika Hospitali  ya rufaa ya mkoa wa Mbeya. 


Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi hufanyika kila mwaka tarehe 12 Mei, ikiadhimisha kuzaliwa kwa Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa